Juzijuzi nilimtebelea rafiki yangu ambaye anajitahidi kuishi kama wale
anaowaona kwenye Luninga, sasa yeye ana kavulana kake kako nasari, nako
anakalea kama vile vitoto vya kwenye Luninga, mwenyewe anakaita junia sijui
junia ndio hivyo hivyo, na kwa vile kule nasari kamejifunza kutamka Dadi and
Mami badala ya baba na mama, jamaa yangu anajiona mjaaaanja, basi Kabwamdogo
hako hakakaripiwi wala kukatazwa chochote.
Nilipata
taarifa kuna siku kalimvua baba yake taulo alipokuwa katoka bafuni tena mbele
za watu, jamaa akaishia kusema tu, "No Junia no...! is bad!? Na kucheka
cheka huku akisifu, "Tatizo la huyu mtoto ni ana akili za kikubwa? Ene wei
siku hiyo jamaa akanikaribisha kwake, basi kwa kweli ilikuwa kero, mara Junia
kaleta mpira anaupiga mbele yetu anaangusha vitu, anatupiga usoni na mpira
anaangaliwa tu, "Junia no!", anapanda meza mara kabati, jamaa yangu
na mke wake utadhani wamelogwa, wanakenua tu meno, "No Junia no" Mara
mbili hivi kakaniparamia na kutaka kunivua miwani yangu, 'Kwa ustaarabu wa
nyumba ile na mie nikatoa ya kinafiki, 'No Junia no'.
Bahati
nzuri mama Junia akaingia jikoni, Baba Junia akaenda chumbani kidogo, sebuleni
tukabaki mimi na hiki kidude kisichokuwa na chembe ya adabu. Si kikaanza
vimaswali vya maudhi...! "Leo umekuja kula kwetu?" "Kwenu mna
TV? Babako anakuleteaga chokoleti?" Kikawa mara kivunje kikombe mara
glasi, mama yake anapiga kelele toka jikoni, "Junia yu a veri bed".
Sasa chenyewe si kikakosea kikanipanda kichwani na kuanza kunivuta nywele
nikaona sasa hii zereu.
Basi
nilikishika mkono nikakitolea macho na kukifinya vizuri mgogongoni. Kwanza
kilitoa macho kama kinataka kufa, kikaniangalia hakiamini akili yake kuwa
kimefinywa na binadamu aliye hai, na mie nikakiambia kwa sauti ya chinichin...
"We Junya ukinisogelea tena nakukata masikio kabisa".
Eeh
bwana we kilitimka mle sebuleni mkojo unakitirirka kikaelekea jikoni. Kufika
huko nilitegemea kianze kulia kwa nguvu, kikawa kimya. Mama yake anakiuliza
"Junia umefanya nini tena baba?" kimya "Junia what has
happened?" kimya, mama yake akaja huku chenyewe kimejificha nyuma ya gauni
la mamake, "Huyu kafanya nini?" Nikajibu kwa sauti ya mtu asiye na
dhambi kabisa... "Wala sijui nimeona tu katimka hapa kaja huko".
Baada
ya hapo kukawa na displin mle ndani tukala na kuzungumza bila fujo. Baba Junia
kila mara akimwangalia mwanae na kumuuliza, "Junia a yu sik?
Unaumwa?" Junia akinitupia jicho mwenyewe alikuwa ananyamaza anajua kuna
kukatwa masikio.
Wengine
hatuangaliagi Luninga ohooo!
No comments:
Post a Comment